WAKATI
wasanii wakubwa wa kimataifa wakiaminika kuwa kioo cha jamii na mfano
bora wa kuigwa na watu wengi, kitendo cha msanii Beyonce Knoweles wa
Marekani kukubali kuwa balozi wa kinywaji cha soda aina ya Pepsi,
kimelaaniwa na kukosolewa na wakereketwa wa masuala ya afya!
Beyonce Knoweles.
Vyakula visivyo na virutubisho (Junk Food) pamoja na vinywaji vyenye
kiwango kingi cha sukari ndivyo vinaaminika kuchangia kwa kiwango
kikubwa ongezekao la magonjwa hatari ya kisukari, shinikizo la damu na
hata kiharusi, na siyo kwa watu wazima tu, bali hata kwa watoto wadogo.
Kwa
mujibu wa mwandishi mahiri wa masuala ya afya wa nchini Marekani, Dk.
Mercola, makampuni makubwa duniani ya vyakula visivyo na lishe bora na
makampuni ya vinywaji baridi, hutumia zaidi za dola za kimarekani
bilioni 2 (zaidi shilingi trioni 3) ku promoti bidhaa zao hatari ili
zitumiwe na watu wakiwemo watoto.
Ingawa jukumu la kuhakikisha mtoto
anakula chakula na kunywa vinywaji bora kwa afya ya binadamu ni la
mzazi, lakini kitendo cha makampuni hayo kutumia wasanii wakubwa kama
Beyonce kwenye matangazo yao, kinaifanya kazi ya wazazi kutekeleza
jukumu lao kuwa ngumu.
Wengi tunapenda kuiga, hasa watoto, vitu
vinavyofanywa na watu maarufu, iwe kwenye chakula na hata muonekanao,
hivyo staa kama Beyonce anapoonekana anatumia soda ya aina fulani, si
rahisi kumkataza mtoto kuitumia soda hiyo, hawezi kukuelewa!
Hivi
karibuni, mwanamuziki huyo ameingia mkataba mnono wa dola za Kimarekani
milioni 50 (zaidi ya bilioni 80 za kibongo) ambazo atalipwa na kampuni
ya Pepsi kwa kuwa balozi wake wa dunia wa kinywaji hicho.
Wakati huku
kwetu kitu chochote kinachopitishwa na wasanii wa kimataifa kinaigwa
kirahisi, hali ni tofauti kwa nchi kama Marekani. Kitendo cha Beyonce
kusaini mkataba huo kimezua mjadala mkubwa kuona baadhi ya wanaojiita
‘mfano mzuri wa kuigwa’ (role models) hawafanyi kwa vitendo vitu
wanavyopaswa kufanya ili kuwa mfano mzuri wa kuigwa na jamii.
Kufuatia taarifa hizo za Beyonce, mtandao wa frugivoremag.com umeandika maoni kadhaa ya kulaani kitendo hicho;
“Wakati
baadhi ya mashabiki wamefurahia mkataba wa Beyonce, wangine wamelaani
kitendo cha kuunga mkono kinywaji chenye sukari ambacho kinachangia
matatizo ya kiafya ya Wamarekani wengi hivi sasa.
“Wengine
wamemtuhumu Beyonce kwa unafiki kwani upande mmoja ameonekana kuungana
na kampeni ya Baraka Obama na mkewe Michelle ya kuwahimiza Wamarekani
kujali afya bora za watoto, wakati upande mwingine anaunga mkono
kinywaji ambacho kinachangia matatizo mengi ya kiafya ya watoto wa
Kimarekani.
“Wakati magonjwa hatari kama Kutetemeka mwili
(Parkinson’s Disease), magonjwa ya moyo, kiharusi na shinikizo la damu
yakiwa yameshamiri duniani, wengine wanalipwa mamilioni ya dola ili
kuimarisha magonjwa hayo,” aliandika pia mtoa maoni mmoja kwenye mtandao
huo.
Utafiti uliyopo kuhusu unywaji wa vinywaji vyenye sukari nyingi
unaonesha kuwa matumizi yote ya vinywaji hivyo yana uhusiano mkubwa na
hatari ya mtu kuongezeka uzito wa mwili na kuwa tipwatipwa, hali ambayo
huongeza hatari ya kupatwa na magonjwa ya kisukari, shinikizo la juu la
damu, na magonjwa ya moyo.
Aidha, kila kinywaji cha ziada chenye
sukari anachotumia mtoto, huongeza uwezekano wa kuongezeka uzito na kuwa
tipwatipwa kwa asilimia 60. Unywaji wa soda kila siku, unaongeza hatari
kwa wanaume ya kupatwa na ugonjwa wa moyo kwa asilimia 19. Unywaji wa
vinywaji viwili au kimoja vyenye sukari kwa siku, huongeza hatari ya mtu
kupatwa na ugonjwa wa kisukari aina ya pili, kwa asilimia 25!
Kimsingi,
makapuni ya vinywaji baridi yanatumia mabilioni ya pesa kila mwaka
kutangaza biashara zao na kuzifanya zionekane hazina madhara kwa
watumiaji, hivyo hatuna budi kuelewa na kukubaliana na ukweli kwamba
vinywaji vyenye sukari, hata kama siyo pombe, ni hatari sana kwa afya
zetu na watoto wetu wako hatarini zaidi.
Tunashauriwa tusiwazoeshe
watoto wetu unywaji wa soda na vinywaji vingine vitamu na badala yake
tuwazoeshe kunywa vinywaji halisi na visivyo na sukari, kama vile juisi
za matunda halisi bila kuweka sukari, maji na vinywaji vingine kama
hivyo. Kama huamini vinywaji baridi ni hatari, jiulize kwa nini hivi
sasa hata watoto wadogo wanaugua ugonjwa wa kisukari na saratani?
Tafakari, chukua hatua!