Mara inasikika sauti iliyozoeleka ya Rais Nyerere
wakati huo ikisema: “Ndugu wananchi, leo majira ya saa 10 jioni, ndugu
yetu, kijana wetu na mwenzetu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Edward Moringe Sokoine wakati akitoka Dodoma kuja Dar es
Salaam, gari yake imepata ajali, amefariki dunia.”
Takribani miaka 29 imepita tangu kufariki kwa,
Edward Moringe Sokoine, aliyepata kuwa waziri mkuu wa Tanzania katika
vipindi viwili tofauti kabla ya kufariki Aprili 12, 1984.
Sokoine alikufa baada ya kutokea ajali ya gari
eneo la Wami-Dakawa, wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro akiwa njiani
kurejea Dar es Salaam akitokea mjini Dodoma alikokuwa akishiriki vikao
vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kumbukumbuka kila mwaka
Aprili 12 ya kila mwaka, taifa limekuwa likiadhimisha kumbukumbu ya kiongozi huyo kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kuendesha makongamano, midahalo, mabonanza, ibada, riadha na upandaji mlima Kilimanjaro.
Aprili 12 ya kila mwaka, taifa limekuwa likiadhimisha kumbukumbu ya kiongozi huyo kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kuendesha makongamano, midahalo, mabonanza, ibada, riadha na upandaji mlima Kilimanjaro.
Katika utawala wa hayati baba wa taifa na rais wa
kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, katika eneo la Wami Sokoine kulijengwa nyumba moja na banda
moja linalotumika kama jukwaa lakini kwa sasa majengo hayo yamechakaa,
anasema msimamizi wa eneo hilo, Hamis Said Mpandachuri.
Mwananchi ilifika katika eneo hilo na kukuta mnara
wa picha ya Sokoine ukiwa umepakwa rangi mpya za manjano, kijani, blue
na nyeusi huku chini ya picha yake kukiwa na maneno “Alimtumikia Mungu
kwa kuwatumikia watu, sauti ya watu ni sauti ya Mungu”.
Mbali ya mnara huo na majengo yaliyojengwa katika
utawala wa serikali ya kwanza, pia liko jengo jipya na la kisasa ambalo
linaendelea kujengwa nyuma ya majengo ya zamani. Kwa mujibu wa uongozi
wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero, jengo hilo ni kwa ajili ya shule ya
sekondari ya Sokoine (Sokoine memorial high school), inajengwa kama
sehemu ya jitihada za wilaya hiyo za kumuenzi Sokoine.
Mbali na jitihada za halmashauri hiyo, Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambacho pia kimebeba jina lake kimekuwa
katika mikakati ya kuhakikisha kuwa kinamuenzi kiongozi huyo kwa kila
hali. Kassim Msagati ni ofisa mawasiliano wa chuo hicho, anasema
hayati, Edward Moringe Sokoine, alikuwa muhimili muhimu wa kuanzishwa wa
chuo kikuu hicho cha kilimo ambacho ni chuo kikuu pekee cha kilimo cha
Serikali nchini.
Aprili 12, 1984 bunge la jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambalo hayati Sokoine alishiriki lilipitisha sheria namba 6 ya
mwaka 1984 ya kuanzishwa kwa chuo kikuu cha kilimo Morogoro. Hapo kabla
chuo hicho kilikuwa ni kitivo cha kilimo cha kilimo na misitu cha chuo
kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Msagati, sheria hiyo iliyopitishwa
na bunge ilikiidhinisha kitivo cha kilimo cha chuo kikuu cha Dar es
salaam kilichokuwa Morogoro kuwa chuo kikuu na kutaka kiitwe chuo kikuu
cha kilimo Morogoro.
Lakini chuo hicho kililazimika kubadilishwa jina
hata kabla ya jina la awali kuanza kutumika na kuitwa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA). Hii ilitokana na kifo cha kiongozi huyo, muda
mfupi baada ya chuo hicho kuidhinishwa rasmi kwa sheria hiyo ambapo
utekelezaji wake ulipaswa kuanza mwezi Julai, 1984, ndipo serikali
ikakubali kiitwe Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo.
No comments:
Post a Comment