Advertise here

Tuesday, February 12, 2013

WANAJESHI WA MALI WAENDELEZA MSAKO MKALI HUKO GAO

Gao
Wanajeshi wa Mali wanafanya msako wa nyumba hadi nyumba kufuatia makabiliano makali na makundi ya wapiganaji wa kiisilamu katika mji wa Gao Jumapili.
Mapigano baina ya wanajeshi wa serikali ya Mali na wapiganaji wa Kiislamu kwa mara ya kwanza yamefika kati-kati ya mji wa Gao, mji mkubwa kabisa kaskazini mwa nchi.
Mwandishi wa BBC aliyeko huko anasema wanajeshi wa Ufaransa wanatumia mizinga dhidi ya wapiganaji hao walioingia hapo kabla.
Anasema ghasia zilianza karibu na makao makuu ya polisi, lakini mapigano yametapakaa. Inaarifiwa baadhi ya wapiganaji wamejificha miongoni mwa wananchi.
Wanajeshi wa Ufaransa na Mali waliukomboa mji huo mwezi uliopita.
Shirika la habari la Ufaransa linaeleza kuwa wapiganaji wa Kiislamu waliovaa nguo nyeusi, huku wamebeba bunduki, waliteka eneo la kati ya mji wa Gao, mji wenye wakaazi wengi kabisa kaskazini mwa Mali.
Wapiganaji hao walipambana na wanajeshi wa Mali leo jioni kwa zaidi ya saa mbili na walionekana wakiranda mitaani kwa pikipiki na wengine walikuwa juu ya mapaa karibu na makao makuu ya polisi.
Karibu na makao hayo wanajeshi wa Mali walitumia makombora na kupambana kwa risasi na washambuliaji ambao wanafikiriwa kuwa wafuasi wa kundi la MUJAO, linalodai kupigana jihadi Afrika Magharibi.
Sauti zilizosikika ni risasi na mbuzi wakikimbia huku wakaazi wa mji wamejificha majumbwani mwao.
Tangu wanajeshi wa Ufaransa kuukomboa mji wa Gao, wapiganaji wa Kiislamu walipambana na wanajeshi nje ya mji lakini hii ndio mara ya kwanza wamefanikiwa kuingia ndani ya mji.

No comments: