Siku
moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza
namba za Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai, katika
mkutano wa hadhara jijini Dar es Salaam, baadhi ya watu wamezitumia
kumtukana Makinda. Chanzo
kilichopo karibu na Spika kimesema kuwa tangu chama hicho kilipotangaza
namba hizo za simu, jumla ya simu 200 za kumtukana Spika zilipigwa.
Hali
kadhalika, katika kipindi hicho jumla ya ujumbe 400 mfupi wa simu za
mkononi (sms), uliokuwa ukimtukana ulipokelewa katika simu zake.
“Simu
hizo walikuwa wameshika wasaidizi wake, kila aliyepiga simu kwa lengo
la kutukana, amekuwa akiachwa kutukana hadi anapomaliza na kisha
kuambiwa sawa,” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake
liandikwe gazetini.
KAULI YA SITTA
Alipoulizwa
kuhusiana na kutukanwa kwa Spika Makinda, Spika Mstaafu, Samuel Sitta,
alisema kumtukana mtu mzima si maadili mema na kwamba hata kama kuna
mambo ambayo mbunge hakubaliani nayo, nchi zote zimeweka taratibu za
kushughulikia mambo kama hayo.
“Wanatakiwa kuwa wavumilivu…wafuate taratibu ambazo zimewekwa katika kushughulikia mambo hayo,” alisema.
Alisema
amesikia kuwa wabunge wa Chadema wakirejea bungeni wameandaa mpango wa
kusimama na kupiga kelele wakati kikao cha Bunge kikiendelea.
“Najiuliza
ni mpango gani kama kupiga kelele, nimesikishwa sana mimi kama mtu
mzima na mambo haya,” alisema Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano
wa Afrika Mashariki.
Kwa
upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema
mambo yanayofanywa na Chadema ni dalili za kufilisika kisiasa.
“Bunge
limeweka taratibu za kushughulika na rufaa na mambo ambayo upande mmoja
unapinga, wao Chadema ndiyo kambi rasmi bungeni wanatakiwa kama kuna
kitu wanakipinga kufuata taratibu zinazokubalika,” alisema.
Aliyekuwa
Mbunge wa Bunge la Tisa kupitia Jimbo la Iramba Magharibi (CCM), Juma
Kilimbah, alisema siyo vibaya kutolewa kwa namba ya simu ya kiongozi,
lakini kama kukiwa na dhamira nzuri.
“Nawatahadharisha
waliopewa wasije wakachuuzwa wakamtukana Spika, maana hii inaweza
kuwasababishia kuwa na kosa la jinai kwa kuwatukana watu,” alisema
Kilimbah, ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya
CCM.
Kwa
mujibu wa viongozi wa Chadema, lengo la kugawa namba hizo za simu ni
kuwataka wananchi ambao waliwaita kuwa ni ‘mahakama ya umma’ wawatumie
ujumbe mfupi wa simu za mkononi wa kuwataka Makinda na Ndugai wajiuzulu
kutokana na kushindwa kuliendesha Bunge kwa kupendelea CCM na kuuonea
upinzani.
Chadema wanadai kuwa kiti cha spika kimekalia rufani za miongozo mingi bila kuitolea majibu tangu mwaka 2011.
Miongoni
mwa ushahidi wa miongozo na rufaa zilizowasilishwa katika ofisi ya
Spika ni ya kiti kwa kukataa kuliwezesha Bunge kujadili hali ya huduma
katika hospitali za umma na jaribio la kutaka kuuawa kwa Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka uliotolewa na Mbunge
wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Nyingine
ni kutoridhishwa na uamuzi wa Naibu Spika wa kukataa mgomo wa walimu na
yatokanayo na mgomo huo kujadiliwa bungeni, malalamiko dhidi ya uamuzi
wa Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Muhagama, kwa kudai kuwa Mnyika anao
ushahidi kuwa Mbunge wa Iramba Magharibi, Lameck Mwigulu Nchemba (CCM),
ni mmoja wa watuhumiwa wa kesi za Epa na kumtaka kuwasilisha ushahidi.
Uamuzi
kuhusiana na uthibitisho kuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
(Chadema), juu ya kauli ya uwongo unaodaiwa kutolewa na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, bungeni wakati akijibu maswali Februari 10, mwaka 2011.
Maamuzi
mengine yanayodaiwa kutotolewa uamuzi na Spika, ni kauli ya Mbunge wa
Meatu (Chadema), Meshack Opulukwa, ambaye alisema bungeni kuwa Mkuu wa
wilaya hiyo, Abihudi Saideya, alihongwa gari ili ampatie mwekezaji
kitalu cha uwindaji kwenye pori la akiba ili wananchi waondolewe eneo
hilo.
Uamuzi
mwingine ambao haujatolewa ni wa Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena
Sakaya (CUF), ambaye alitakiwa kuwasilisha uthibitisho wa kauli yake
kuwa Mkuu wa Wilaya ya Urambo, aliingia katika zizi la mfugaji na kutoa
mbuzi kisha kumchinja bila ridhaa ya mmiliki.
Uamuzi
mwingine ni mwongozo wa kuhusu kauli ya Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu, ambaye alisema kuwa majaji wengi wanateuliwa
bila kuwa na sifa.
Mwongozo
mwingine ambao haujatolewa maamuzi licha ya kuwasilishwa kwa ushahidi,
ni Baraza la Mawaziri kushawishi Shirika Hodhi la Mashirika ya umma
(CHC) lisiongezewe mkataba.
Viongozi
wa Chadema waligawa namba za viongozi hao wa juu wa Bunge Jumapili
iliyopita katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya
Temeke Mwisho, jijini Dar es Salaam.
NDUGAI AWAJIBU CHADEMA
Kufuatia
shinikizo hilo, Ndugai amesema kuwa Chadema wanapaswa kufuata kanuni na
sheria zilizomo katika katiba za kuwaondoa madarakani viongozi kuliko
kutumia njia ya maandamano.
Akuzungumza
jana kwa njia ya simu kuhusiana na alivyopokea wito wa Chadema wa
kumtaka aachie ngazi, Ndugai alisema kuna sheria na taratibu zilizowekwa
katika kuiongoza nchi, hivyo kila mtu anapaswa kuzifuata.
Alisema
endapo Mbunge akimtaka rais, waziri, spika au kiongozi yeyote aliyeko
serikalini kujiuzulu, inampasa kufuata utaratibu uliowekwa na siyo
kutumia njia ya maandamano.
Ndugai
alisema mbunge pia anaweza kuandika barua au kuwasilisha hoja bungeni
ya kumtaka spika au naibu spika ajiuzulu na hoja hiyo itajadiliwa na
wabunge.
“Wanapaswa
kuwasilisha hoja bungeni, hoja itapokelewa lakini, siyo kwa njia ya
maandamano, ile ni ofisi ya umma siyo yangu, kila mtu ana haki ya
kuliongoza Bunge,” alisema Ndugai, ambaye alilalamikiwa na upinzani kwa
hatua yake ya kukubali Bunge liondoe hoja ya Mbunge wa Kuteuliwa, James
Mbatia (NCCR-Mageuzi) kuhusu kasoro katika mtaala wakati wa Mkutano wa
10 uliomalizika wiki iliyopita