Advertise here

Tuesday, January 15, 2013

Simba Full Muziki



Simba wakiwa kwenye mazoezi yao nchini Oman
DORIS MALIYAGA, OMAN
SIMBA sasa wapo kamili. Baada ya kutua kwa nyota wake waliokuwa Taifa Stars na Kombe la Mapinduzi Zanzibar kumekamilisha kikosi chake kilichopiga kambi hapa Muscat, Oman.

Wachezaji watatu Amir Maftah, Edward Christopher na Mussa Mudde ndio wachezaji ambao hawajajiunga na kambi ya Simba hapa Oman kutokana na sababu mbalimbali.

Meneja wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo alisema kila mmoja amebaki kutokana na sababu zake.

"Maftah amebaki kwa tatizo la nidhamu, Mudde amepata matatizo ya kifamilia yuko kwao Uganda."

Christopher, hata hivyo, amebakizwa baada ya kuumia kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Maftah alitakiwa kutua jana Jumatatu na wenzake waliokuwa Taifa Stars lakini alizuiwa kuondoka kutokana na utovu wa nidhamu, ambao haukuwekwa wazi na Julio.

Simba inajifua vilivyo tangu walipofika Januari 9, ingawa walifika kwa mafungu tofauti.

Walianza wakiwa na wachezaji nane, wakaongezeka kufikia 13 na sasa wametimia 24.

Nyota walioko Oman ni pamoja na Juma Kaseja, Ramadhani Chombo 'Redondo', Haruna Moshi, Boban', Mzambia Felix Sunzu, Said Nassor 'Cholo', Haruna Shamte, Haruna Chanongo, Kigi Makassy, Abdallah Seseme, Ramadhan Singano, Mrisho Ngassa na Mwinyi Kazimoto.

Wengine ni Abdallah Juma, Paul Ngalema, Amri Kiemba, Shomari Kapombe, Abel Dhaira na baadhi kutoka timu ya yosso ya Simba.

Kocha mkuu wa kikosi hicho, Mfaransa Patrick Liewig amesema lengo lake na tabia yake kama dereva ni kuhakikisha Simba inakuwa timu nzuri.

�Tunatakiwa kufanya kazi ili tufanikiwe ambapo sasa natengeneza timu ya ushindi tu.�

Viwanja tofauti
Simba inafanya mazoezi katika viwanja vitatu. Kuna siku inafanya kwenye uwanja wa klabu ya Fanja.

Mara nyingine wanajifua katika Uwanja wa Klabu ya Michezo inayoitwa Oman.

Simba pia imefanya mazoezi katika Uwanja wa Michezo wa Sultan Qaboos, ambao unamilikiwa na serikali ya hapa.

Total Football
Kocha Liewig amesisitiza kitu anachokifanya sasa ni kutengeneza timu yenye kushirikiana ambayo itashambulia pamoja na kuzuia pamoja lakini pia iwe inafunga mabao.

Staili hiyo kwa jina la kimombo huitwa `Total Football�, ambayo ilikuwa inachezwa zaidi na timu za Uholanzi kwenye miaka ya 1970.

Pengine hiyo ni janja ya Liewig kuanza kusuka mbinu za kuidhibiti Yanga, ambayo inanolewa na Mholanzi Ernest Brandt.

Kumbuka Brandt alikuwemo katika kikosi cha timu ya taifa Uholanzi kilichotikisa na staili hiyo chini ya kocha Rinus Michel.

�Muhimu ninachokifanya ni kutengeneza kombinesheni ya timu. Nilikuwa Zanzibar na nimeiona timu ikicheza nimegundua upungufu hasa katika ushambuliaji na kujihami.�

Nataka mambo yafanywe na timu kwa pamoja kwani yatasaidia kuongeza ushirikiano wa wachezaji na timu kuwa ngumu kufungika.

Sunzu, Kazimoto waugua
Sunzu alikatiza mazoezi ya jana Ijumaa jioni baada ya kufanya kwa nusu saa. Alikimbizwa hospitali na aligundulika alikuwa na tatizo la kifua.

Hata hivyo, kitendo hicho cha kukatiza mazoezi na kulalamika kujisikia vibaya kuliwatia hofu watu pengine tatizo lake la moyo lilikuwa limerudi.

Sunzu alitaka kukatiza mkataba na Simba kwenye Dirisha Dogo la usajili kwa madai alikuwa ana tatizo la moyo.

Ingawa baada ya muda alibadili mawazo na kurudi nchini na kujiunga na Simba tena.

Kipa Dhaira naye alipelekwa hospitali baada ya kufanya mazoezi ya asubuhi. Pia naye alikuwa na tatizo la kifua na alipewa dawa.

Kazimoto hakufanya kabisa mazoezi na aligundulika alikuwa na malaria.

Sunzu na Boban
Liewig anaeleza kuwa anataka Sunzu na Boban ndio waongoze safu ya ushambuliaji.

�Nimeanza na hawa kwa kuwa ndio nilikuwa nao kwa kipindi chote kwa sasa wamekuja hawa wengine mambo yatakuwa mazuri zaidi naweza kuamua namna gani nitakavyowachezesha,� alieleza Liewig.

Mfaransa huyo anaona nyota hao wawili wanaweza kutengeneza safu kali ya ushambuliaji.

Kocha huyo amefurahia ujio wa wachezaji wote lakini amesisitiza muda wa siku 10 uliobaki ni mfupi kwa maandalizi yake.

Simba walikiwa na idadi kubwa ya wachezaji walifanya mazoezi jana Jumatatu katika Uwanja wa Oman na walianza kwa mazoezi ya kukimbia chini ya Julio.

Katika mazoezi hayo walifanya ya ufundi kwa kucheza pasi ndefu na fupi ambapo kocha amesisitiza lengo ni umakini kwa
mchezaji anapokuwa na mpira kwa kutoa pasi na kupokea.

No comments: