Advertise here

Tuesday, January 15, 2013

BEYONCE ALAANIWA KWA KUISHABIKIA SODA!

WAKATI wasanii wakubwa wa kimataifa wakiaminika kuwa kioo cha jamii na mfano bora wa kuigwa na watu wengi, kitendo cha msanii Beyonce Knoweles wa Marekani kukubali kuwa balozi wa kinywaji cha soda aina ya Pepsi, kimelaaniwa na kukosolewa na wakereketwa wa masuala ya afya!
Beyonce Knoweles.
Vyakula visivyo na virutubisho (Junk Food) pamoja na vinywaji vyenye kiwango kingi cha sukari ndivyo vinaaminika kuchangia kwa kiwango kikubwa ongezekao la magonjwa hatari ya kisukari, shinikizo la damu na hata kiharusi, na siyo kwa watu wazima tu, bali hata kwa watoto wadogo.
Kwa mujibu wa mwandishi mahiri wa masuala ya afya wa nchini Marekani, Dk. Mercola, makampuni makubwa duniani ya vyakula visivyo na lishe bora na makampuni ya vinywaji baridi, hutumia zaidi za dola za kimarekani bilioni 2 (zaidi shilingi trioni 3) ku promoti bidhaa zao hatari ili zitumiwe na watu wakiwemo watoto.
Ingawa jukumu la kuhakikisha mtoto anakula chakula na kunywa vinywaji bora kwa afya ya binadamu ni la mzazi, lakini kitendo cha makampuni hayo kutumia wasanii wakubwa kama Beyonce kwenye matangazo yao, kinaifanya kazi ya wazazi kutekeleza jukumu lao kuwa ngumu.
Wengi tunapenda kuiga, hasa watoto, vitu vinavyofanywa na watu maarufu, iwe kwenye chakula na hata muonekanao, hivyo staa kama Beyonce anapoonekana anatumia soda ya aina fulani, si rahisi kumkataza mtoto kuitumia soda hiyo, hawezi kukuelewa!
Hivi karibuni, mwanamuziki huyo ameingia mkataba mnono wa dola za Kimarekani milioni 50 (zaidi ya bilioni 80 za kibongo) ambazo atalipwa na kampuni ya Pepsi kwa kuwa balozi wake wa dunia wa kinywaji hicho.
Wakati huku kwetu kitu chochote kinachopitishwa na wasanii wa kimataifa kinaigwa kirahisi, hali ni tofauti kwa nchi kama Marekani. Kitendo cha Beyonce kusaini mkataba huo kimezua mjadala mkubwa kuona baadhi ya wanaojiita ‘mfano mzuri wa kuigwa’ (role models) hawafanyi kwa vitendo vitu wanavyopaswa kufanya ili kuwa mfano mzuri wa kuigwa na jamii.
Kufuatia taarifa hizo za Beyonce, mtandao wa frugivoremag.com umeandika maoni kadhaa ya kulaani kitendo hicho;
 “Wakati baadhi ya mashabiki wamefurahia mkataba wa Beyonce, wangine wamelaani kitendo cha kuunga mkono kinywaji chenye sukari ambacho kinachangia matatizo ya kiafya ya Wamarekani wengi hivi sasa.
“Wengine wamemtuhumu Beyonce kwa unafiki kwani upande mmoja ameonekana kuungana na kampeni ya Baraka Obama na mkewe Michelle ya kuwahimiza Wamarekani kujali afya bora za watoto, wakati upande mwingine anaunga mkono kinywaji ambacho kinachangia matatizo mengi ya kiafya ya watoto wa Kimarekani.
“Wakati magonjwa hatari kama Kutetemeka mwili (Parkinson’s Disease), magonjwa ya moyo, kiharusi na shinikizo la damu yakiwa yameshamiri duniani, wengine wanalipwa mamilioni ya dola ili kuimarisha magonjwa hayo,” aliandika pia mtoa maoni mmoja kwenye mtandao huo.
Utafiti uliyopo kuhusu unywaji wa vinywaji vyenye sukari nyingi unaonesha kuwa matumizi yote ya vinywaji hivyo yana uhusiano mkubwa na hatari ya mtu kuongezeka uzito wa mwili na kuwa tipwatipwa, hali ambayo huongeza hatari ya kupatwa na magonjwa ya kisukari, shinikizo la juu la damu, na magonjwa ya moyo.
Aidha, kila kinywaji cha ziada chenye sukari anachotumia mtoto, huongeza uwezekano wa kuongezeka uzito na kuwa tipwatipwa kwa asilimia 60. Unywaji wa soda kila siku, unaongeza hatari kwa wanaume ya kupatwa na ugonjwa wa moyo kwa asilimia 19. Unywaji wa vinywaji viwili au kimoja vyenye sukari kwa siku, huongeza hatari ya mtu kupatwa na ugonjwa wa kisukari aina ya pili, kwa asilimia 25!
Kimsingi, makapuni ya vinywaji baridi yanatumia mabilioni ya pesa kila mwaka kutangaza biashara zao na kuzifanya zionekane hazina madhara kwa watumiaji, hivyo hatuna budi kuelewa na kukubaliana na ukweli kwamba vinywaji vyenye sukari, hata kama siyo pombe, ni hatari sana kwa afya zetu na watoto wetu wako hatarini zaidi.
Tunashauriwa tusiwazoeshe watoto wetu unywaji wa soda na vinywaji vingine vitamu na badala yake tuwazoeshe kunywa vinywaji halisi na visivyo na sukari, kama vile juisi za matunda halisi bila kuweka sukari, maji na vinywaji vingine kama hivyo. Kama huamini vinywaji baridi ni hatari, jiulize kwa nini hivi sasa hata watoto wadogo wanaugua ugonjwa wa kisukari na saratani?
Tafakari, chukua hatua!

No comments: