Advertise here

Friday, April 12, 2013

YA KUKUMBUKWA MIAKA 29 KIFO CHA SOKOINE

Ilikuwa Jumatano ya Aprili 12, 1984 saa 11:30 jioni, siku ambayo Dar es Salaam ilinyesha mvua kutwa nzima. Wakati kipindi cha salaam cha Jioni Njema cha Redio Tanzania (RTD) wakati huo kikiwa hewani, mara matangazo yake yanakatishwa ghafla na wimbo wa taifa unapigwa.
Mara inasikika sauti iliyozoeleka ya Rais Nyerere wakati huo ikisema: “Ndugu wananchi, leo majira ya saa 10 jioni, ndugu yetu, kijana wetu na mwenzetu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine wakati akitoka Dodoma kuja Dar es Salaam, gari yake imepata ajali, amefariki dunia.”
Takribani miaka 29 imepita tangu kufariki kwa, Edward Moringe Sokoine, aliyepata kuwa waziri mkuu wa Tanzania katika vipindi viwili tofauti kabla ya kufariki Aprili 12, 1984.
Sokoine alikufa baada ya kutokea ajali ya gari eneo la Wami-Dakawa, wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro akiwa njiani kurejea Dar es Salaam akitokea mjini Dodoma alikokuwa akishiriki vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kumbukumbuka kila mwaka
Aprili 12 ya kila mwaka, taifa limekuwa likiadhimisha kumbukumbu ya kiongozi huyo kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kuendesha makongamano, midahalo, mabonanza, ibada, riadha na upandaji mlima Kilimanjaro.
Katika utawala wa hayati baba wa taifa na rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika eneo la Wami  Sokoine kulijengwa nyumba moja na banda moja linalotumika kama jukwaa lakini kwa sasa majengo hayo yamechakaa, anasema msimamizi wa eneo hilo, Hamis Said Mpandachuri.
Mwananchi ilifika katika eneo hilo na kukuta mnara wa picha ya Sokoine ukiwa umepakwa rangi mpya za manjano, kijani, blue na nyeusi huku chini ya picha yake kukiwa na maneno “Alimtumikia Mungu kwa kuwatumikia watu, sauti ya watu ni sauti ya Mungu”.
Mbali ya mnara huo na majengo yaliyojengwa katika utawala wa serikali ya kwanza, pia liko jengo jipya na la kisasa ambalo linaendelea kujengwa nyuma ya majengo ya zamani. Kwa mujibu wa uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero, jengo hilo ni kwa ajili ya shule ya sekondari ya Sokoine (Sokoine memorial high school), inajengwa kama sehemu ya jitihada za wilaya hiyo za kumuenzi Sokoine.
Mbali na jitihada za halmashauri hiyo, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambacho pia kimebeba jina lake kimekuwa katika mikakati ya kuhakikisha kuwa kinamuenzi kiongozi huyo kwa kila hali. Kassim Msagati ni ofisa mawasiliano wa chuo hicho,  anasema hayati, Edward Moringe Sokoine, alikuwa muhimili muhimu wa kuanzishwa wa chuo kikuu hicho cha kilimo ambacho ni chuo kikuu pekee cha kilimo cha Serikali nchini.
Aprili 12, 1984 bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo hayati Sokoine alishiriki lilipitisha sheria namba 6 ya mwaka 1984 ya kuanzishwa kwa chuo kikuu cha kilimo Morogoro. Hapo kabla chuo hicho kilikuwa ni kitivo cha kilimo cha kilimo na misitu cha chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Msagati, sheria hiyo iliyopitishwa na bunge ilikiidhinisha kitivo cha kilimo cha chuo kikuu cha Dar es salaam kilichokuwa Morogoro kuwa chuo kikuu na kutaka kiitwe chuo kikuu cha kilimo Morogoro.
Lakini chuo hicho kililazimika kubadilishwa jina hata kabla ya jina la awali kuanza kutumika na kuitwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). Hii ilitokana na kifo cha kiongozi huyo, muda mfupi baada ya chuo hicho kuidhinishwa rasmi kwa sheria hiyo ambapo utekelezaji wake ulipaswa kuanza mwezi Julai, 1984, ndipo serikali ikakubali kiitwe Chuo Kikuu cha Sokoine cha kilimo.

No comments: