Advertise here

Monday, February 04, 2013

MADUKA YATEKETEA KWA MOTO MWENGE

Hivi ndivyo eneo la Mwenge kituoni lilivyokuwa majira ya saa tano asubuhi ambapo shughuli zote ikiwemo usafiri wa Daladala kuelekea katikati ya Jiji na maeneo mengine zilisimama ili kupisha vikosi vya Zima Moto na Uokoaji vya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuzima moto uliokuwa ukiteketeza baadhi ya maduka.
Licha ya Moto huo kuonesha kuwa na madhara zaidi, vikosi vya zimamoto vikishirikiana na vile vya Kampuni binafsi za Ulinzi vilifanikiwa kuuzima moto huo na kupunguza hatari ya kuhamia kwenye maduka mengine ambayo yamekaribiana.
Akizungumzia tukio, Mkuu wa Ulinzi Shirikishi Kituo cha Mabasi Mwenge KESSY MLUGURU amesema, waligundua kutokea kwa moto huo katika moja ya duka majira ya saa tatu asubuhi na kuanza juhudi za kuuzima kwa maji yakiyo kwenye tenki ambapo Mkuu wa Kituo cha Polisi Mabatini Kijitonyama anathibitisha kutokea kwa moto huo.
Mmoja ya Wamiliki wa maduka ya vipodozi ambayo yameteketea MAPINDUZI WILSON amesema, moto huo umetokea kutokana na hitilafu ya umeme iliyotokea kwenye moja ya waya zinazoingia kwenye maduka hayo.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, Meja KURWA NZELEKELA amesema kikosi chake kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo miundombinu ya barabarani na usalama wanapokuwa kazini.
Tukio hili linafuatiwa na lile lililotokea jana kwenye Jengo la PPF TOWER lililopo Makutano ya Mtaa wa Ohio na Garden kunusurika kuteketea kwa moto baada ya moja ya ghorofa zake kushika moto ambao pia ulidhibitiwa na vikosi hivyo vya zima moto.

No comments: